Makala ya Jamii

Jukwaa Tendaji la Laudato Si’ Lazinduliwa

Posted 7 June 2021

Kadinali Peter Turkson (picha, Mazur/catholicnews.org.uk)

Kadinali Peter Turkson, Kiranja wa Wizara ya Ukuzaji wa Maendeleo Muhimu ya Kibinadamu, Vatikani, ametangaza kubuniwa kwa Jukwaa Tendaji la Laudato Si’

Jukwaa Tendaji la Laudato Si’ ni mradi wa msingi katika kuliimarisha Kanisa la Ulimwnegu ili kutimiza uhimilivu kamili kwa dhati ya moyo wa ikolojia fungamano. Huku wanadamu wakizidi kukabiliana dhidi ya migogoro ya kiikolojia, Jukwaa Tendaji la Laudato Si’ linatoa mwongozo mpya, kuwaunganisha Wakatoliki na wote wa nia njema kwenye harakati za kutimiza mustakabali wa haki na ulio stahimilivu. 

Jukwaa Tendaji la Laudato Si’ hujikita kwenye msingi ulioasisiwa na makundi ya washirika.  Katika kubuni fursa za kuchanga bia, linatoa nguvu-mwendo mpya ili kuishughulikia kwa dharura na kwa moyo wa matamanio migogoro ya kiikolojia. 

Tangazo la leo linasadifu na kufungwa kwa Juma la Laudato Si’ na Mwaka wa Maadhimisho Maalum ya Laudato Si’

Padre. Joshtrom Kureethadam, Mratibu wa Idara ya Wizara ya Ikolojia, aliandamana na Kadinali Turkson katika hafla ya matangazo rasmi. 

Padre Kurrethadam alisema, “ Jukwaa Tendaji la Laudato Si’, huitekeleza kimatendo ndoto yake Baba Mtakatifu Fransisko ya kuukusanya pamoja umati wa watu kuanzia matabaka ya chini kwa ajili ya kuyatunza makao yetu sote. Huwakilisha juhudi za kujifundisha na kuzitia shime jamii ambazo zinaongoza jitihada za Laudato Si’ duniani kote. Yakini, kunayo mifano ya uongozi wenye kariha na wa  kutumainisha kutoka idara zote saba zinazohudumiwa na programu hii. Matumaini yetu ni kuwa jukwaa litatoa nafasi na satua sawa kwa wote ili kuungana na kukua pamoja.” 

Padre Kureethadam aliendelea na kusema, “ Muungano wa washirika ambao wanaongoza harakati hizi pamoja na Wizara ni wa kupigiwa mfano. Uwezo na nguvu tulizo nazo kwenye programu hii kufikia sasa, pakubwa,  ni kwa ajili ya ukarimu wao katika uongozi na hekima zao. Kwa kweli, tunatazamia kwa utegemezi viongozi hawa kindakindaki kwa maarifa yao na ubingwa ambavyo ni kiini muhimu katika kulihudumia Kanisa la Ulimwengu.” 

Padre Kureethadam alihitimisha kwa kusema, “ Jukwaa Tendaji la Laudato Si’ linatoa mwongozo mpya huku tukitamatisha Maadhimisho ya Mwaka Maalum wa Laudato Si’ wa Baba Mtakatifu Fransisko na kuingia katika hatua zijazo za safari yetu. Tunakualikeni nyote tuungane alimradi kuyajenga maisha yetu bora ya usoni kwa pamoja. Tutembee pamoja! Hii ni jamii ya Kanisa la Sinodi ambayo Papa Fransisko anatualika kuiunda huku tukizidi kuyatunza makao tunayoshiriki sote na sisi wenyewe kwa wenyewe.”